Wanne wakamatwa na EACC kwa madai ya kupokea hongo

KBC Digital News
3 Min Read

 Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewakamata maafisa wanne wa umma katika operesheni tofauti katika kaunti za Kwale na Bungoma.

Wanne hao walijipata wakikwaruzana na mkono mrefu wa sheria kwa madai ya kuitisha na kupokea hongo kutoka kwa wananchi.

Waliokamatwa ni maafisa wawili wa usalama wa kampuni ya Kenya Power mjini Diani, Kaunti ya Kwale, na maafisa wawili wa uzingatiaji sheria na utekelezaji wa kanuni katika serikali ya kaunti ya Bungoma, mjini Kimilili.

Huko Kwale, maafisa wa EACC kutoka Ofisi ya Kanda ya Pwani ya Chini, Mombasa, waliwakamata maafisa wa Kenya Power Joseph Dena na Fredrick Odhiambo baada ya kudaiwa kuitisha hongo ya shilingi 100,000 kutoka kwa mlalamishi.

Maafisa hao wanadaiwa kumshutumu mlalamishi kwa kutumia umeme kinyume cha sheria na kumtaka awape fedha hizo ili wamsaidie kuachiliwa na kuhakikisha kuwa hachukuliwi hatua za kisheria.

Baada ya kupokea malalamishi hayo, EACC iliendesha operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa washukiwa hao walipokuwa wakipokea shilingi 50,000.

Walifikishwa katika kituo kikuu cha polisi mjini Mombasa kuandikisha taarifa na baadaye wakaachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya shilingi 20,000 kila mmoja huku uchunguzi ukiendelea.

Na huko Bungoma, maafisa wa EACC  waliwakamata askari wa serikali ya kaunti, Victoria Mala Nafula na Elizabeth Nafuna Lukhale, baada ya kudaiwa kuitisha na kupokea hongo kutoka kwa mhudumu wa cyber café katika manispaa ya Kimilili.

Maafisa hao wanadaiwa kumtaka mfanyabiashara huyo awape fedha hizo ili amruhusu kuendelea kuendesha biashara yake bila leseni. Pia wanadaiwa kumtishia kufunga biashara hiyo iwapo hangewapa hongo hiyo.

Baada ya uchunguzi wa awali, EACC iliendesha operesheni na kuwakamata maafisa hao walipokuwa wakipokea pesa kutoka kwa mlalamishi.

Washukiwa hao walipelekwa katika Ofisi ya EACC, Kanda ya Magharibi mjini Bungoma kuandikisha taarifa, na baadaye wakapelekwa katika kituo cha polisi cha Bungoma, ambako walilala usiku mmoja.

Waliachiliwa asubuhi kwa dhamana ya shilingi 20,000 pesa taslimu kila mmoja huku uchunguzi ukiendelea.

Kukamatwa kwa maafisa hao kunajiri wakati tume hiyo inaongeza juhudi za kukabiliana na hongo na aina zingine za ufisadi katika vituo vya utoaji huduma, ambako wananchi hukutana moja kwa moja na maafisa wa umma.

Share This Article