Aliyekuwa Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu ya Nairobi Nzioka Waita amemshutumu Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti kwa kuvamia majengo ya bunge la kaunti hiyo jana Jumatatu.
Wavinya alivamia bunge hilo kulalamikia mabadiliko yaliyofanywa kwenye Mswada wa Bajeti yenye kima cha shilingi bilioni 17.8.
Wavinya analitaka bunge hilo kuzingatia upya mswada huo, akiwatuhumu wawakilishi wadi kwa kubadilisha mipango ya matumizi ya kaunti hiyo na kupunguza au kuelekeza fedha kwingineko kinyume cha sheria.
“Kuvamia majengo ya bunge na wahuni, na kuwanyanyasa maafisa wa bunge hilo, siyo huduma ya mkataba. Ni shambulizi dhidi ya heshima ya bunge na usalama binafsi wa watumishi wa umma,” alisema Nzioka kwenye taarifa.
Nzioka sasa anatoa wito kwa Huduma ya Taifa ya Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kumchunguza Gavana huyo na kumchukulia hatua ikiwa atapatikana na hatia.
Ukosoaji wa Nzioka unakuja wakati wawili hao wanatarajiwa kutoana kijasho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Huku Wavinya akitarajiwa kutetea kiti hicho kwa chama cha Wiper, Nzioka anatafuta kumbandua madarakani kwa chama cha UDA.
Wavinya alimbwaga Nzioka kwenye uchaguzi mkuu uliopita na kuchaguliwa Gavana mpya wa Machakos.