Mama Rachel asisitiza umuhimu wa kuwalinda watoto

Martin Mwanje
2 Min Read
Mama Rachel Ruto akiwa na viongozi wengine wakati wa kongamano la vijana Homa Bay

Mama Taifa Rachel Ruto amesisitiza umuhimu wa watu wazima kuchukua jukumu ongozi la kuwalinda watoto katika jamii. 

Hususan, ametaka mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi, mimba za mapema, na dhuluma za kijinsia na kingono kuchukuliwa kama suala la dharura ili kuwalinda watoto na ndoto zao.

Akizungumza wakati wa kongamano la vijana katika kaunti ya Homa Bay, Mama Rachel alitaja hiyo kuwa sababu iliyomfanya kuzindua kampeni ya kitaifa ya kutokomeza matishio hayo yanayojulikana kama Triple Threat chini ya mpango wa dhamira wa mwaka 2023-2030.

Mpango huo ulianzishwa katika kaunti za Meru na Narok na kisha kuelekezwa katika kaunti za Homa Bay, Samburu, West Pokot na Uasin Gishu.

“Ndani ya miezi sita, vituo vya afya zaidi ya 220 vimejiunga na mpango huo katika kaunti hizo nne, na zaidi ya wahudumu wa afya zaidi ya 200 kupewa mafunzo ya kutoa huduma rafiki kwa vijana waliobalehe,” alisema Mama Rachel.

“Sasa hiki ni kipaumbele cha kitaifa, kwa sababu dhamira yetu lazima iwe bayana: kumaliza Triple Threat kufikia mwaka 2027. Lakini lazima tuwe wawazi: Kampeni peke yake haitalinda watoto wetu.”

Alitoa wito wa ushirikiano wa wadau wote wakiwemo walimu, wazazi, wahudumu wa afya, machifu na jamii yote kwa jumla.

“Kwa vijana wetu, salia shuleni, linda ndoto zako, na kitu kinapoenda mrama, zungumza. Mwambie Mwalimu.  Mzazi. Mhudumu wa afya. Mtu unayemwamini,” aliongeza Mama Rachel.

“Usiruhusu mtu kukushawishi kwamba siku zako za usoni ni gharama unayopaswa kulipa ili kupata pesa, kukubaliwa au kupendwa. Siku zako za usoni ni zako. Na ndoto zako zinastahili kulindwa.”

Share This Article