Rais Ruto amwomboleza mkewe Khalwale

Aliahidi kusimama na Seneta Khalwale na familia yake katika kipindi hiki kigumu cha majonzi makubwa.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto na mkewe Rachel wamemwomboleza Gloria Sekeiyan, mke wa Seneta wa kaunti ya Kakamega Bonny Khalwale aliyefariki hapo jana.

“Mama Rachel nami tunatoa salamu zetu za dhati za pole kwa Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, kufuatia kifo cha mke wake mpendwa, Gloria Sekeiyan” alisema kiongozi wa nchi katika ufunguzi wa taarifa yake.

Aliahidi kusimama na Seneta Khalwale na familia yake katika kipindi hiki kigumu cha majonzi makubwa.

Ruto aliendelea kusema kwamba Kupoteza mwenzi wa maisha, mshirika na mama huacha pengo kubwa moyoni akiongeza, “Tunaomba Mungu awajalie familia nguvu, faraja na amani wanapomlilia na kutunza kumbukumbu yake”.

Gloria Sekeiyan Khalwale, alifariki dunia jana asubuhi baada ya kuanguka ghafla kufuatia kile kinachoshukiwa kuwa mshtuko wa moyo.

Khalwale alithibitisha kifo hicho kupitia taarifa, akisema alifariki Jumamosi asubuhi.

Alifichua kuwa Sekeiyan alikuwa mama wa watoto wao wanane lakini hakufichua iwapo marehemu mke wake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wowote kabla ya kifo chake cha ghafla.

Viongozi kadhaa wa kisiasa wamekuwa wakitoa jumbe za pole kwa Seneta Khalwale akiwemo Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliyeandika, “Omwami Khalwale, pole sana kwa msiba wako. Mungu akufariji wewe na familia yako katika kipindi hiki kigumu”.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Bunge la Kitaifa, Samuel Atandi, pia alituma rambirambi zake kwa Khalwale na familia yake.

“Pole sana, Seneta. Mungu akufariji wewe na familia yako katika kipindi hiki kigumu,” Atandi alisema.

Share This Article