Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amewaonya maafisa wa polisi dhidi ya kujihusisha na shughuli za kisiasa au kutumiwa na wanasiasa katika kutekeleza maslahi yao binafsi.
Kanja amesema maafisa wa polisi wakati wote wanapaswa kutopendelea upande wowote wa kisiasa na kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia Katiba na sheria za nchi.
Akizungumza katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo, Kaunti ya Nyeri, wakati wa hafla ya kufuzu kwa makurutu wa polisi, Kanja pia alikemea visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa maafisa wa polisi.
Alisema maafisa watakaobainika kukiuka kanuni za utumishi au kujihusisha na vitendo vinavyokiuka sheria watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
Wakati huo huo, Kanja amesema Huduma ya Kitaifa ya Polisi inaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuboresha utendaji wake na kuimarisha utoaji wa huduma kwa umma.
Miongoni mwa hatua hizo ni uzinduzi wa sare mpya za polisi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Inspekta Mkuu huyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa maafisa na kuimarisha huduma ya polisi kwa Wakenya.
Kanja amesisitiza kuwa nidhamu, uadilifu na uweledi ni nguzo muhimu katika kujenga huduma ya polisi inayozingatia sheria na inayoweza kuaminika na wananchi.
Taarifa ya William Khaemba