Wamiliki wa Vyombo vya Habari waomboleza waliofariki ajali ya helikopta

Saba hao walifariki katika ajali ya helikopta iliyotokea katika kaunti ya Samburu mapema Agosti 19.

Martin Mwanje
2 Min Read
Agnes Kalekye - Mwenyekiti wa MOA

Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini, MOA wametuma risala za rambirambi kufuatia vifo vya watu saba katika ajali ya helikopta iliyotokea mapema jana Jumatano. 

Ajali hiyo ilitokea katika vilima vya Sapache karibu na Mlima Ololokwe huko Samburu Mashariki.

Hususan, MOA imeelezea kusikitishwa mno na kifo cha Jose Alberto Suarez ambaye alikuwa Rais na Meneja Mkuu wa vituo vya Telemundo huko Orlando, Tampa, na Fort Myers-Naples huko Florida.

“Mtendaji wa vyombo vya habari kwa zaidi ya miongo miwili katika vituo vinavyomilikiwa na Telemundo na NBC, ushawishi wake ulienea nje ya Marekani,” alisema Agnes Kalekye, Mwenyekiti wa MoA ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji nchini, KBC.

“Vituo vyetu wanachama vimepeperusha maudhui ya Telemundo miaka iliyopita, na kuleta vipindi alivyosaidia kuvitengeneza katika makazi nchini Kenya. Kwa namna hiyo, kazi yake ilijenga daraja kimyakimya kati ya ulimwengu wetu wa vyombo vya habari.”

Kwenye taarifa, Kalekye amewaomboleza wote waliofariki kwenye ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 3:13 asubuhi.

Wengine waliofariki ni Josh Outran ambaye alikuwa rubani, Roger Duarte, Adam Navaty na Stephen Vascanknez.

Wengine ni Henry Parra na Michael Contugi.

Maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu ni miongoni mwa waliofika eneo la ajali kusaidia katika jitihada za uokozi.

Mamlaka nchini Kenya zinachunguza chanzo cha ajali hiyo.

Share This Article