Mwanamuziki mashuhuri wa asili ya Benin, Angélique Kidjo, ambaye ameshinda tuzo tano za Grammy, ameweka historia baada ya kutunukiwa nyota kwenye Hollywood Walk of Fame.
Kwa nyota hiyo nambari 2,854 ameweka historia ya kuwa mwanamuziki wa kwanza kutoka Afrika na msanii wa kwanza Mwafrika mweusi kuwahi kupata heshima hiyo ya kifahari.
Kidjo alitunukiwa heshimiwa hiyo jana Jumanne, Agosti 18, 2026, huko Hollywood Boulevard, Los Angeles, mkabala na Hoteli ya Hollywood Roosevelt.
Hafla hiyo ilifanyika saa tano unusu asubuhi, saa za Pacific, na kumtambua katika kitengo cha kurekodi, huku ikiadhimisha safari yake ya zaidi ya miongo minne katika muziki.
Muigizaji Willem Dafoe na Mkurugenzi Mtendaji wa Akademia ya kurekodi inayosimamia masuala hayo, Harvey Mason Jr. ni miongoni mwa wageni waliozungumza kwenye hafla hiyo, iliyosisitiza mchango mkubwa wa Kidjo katika muziki na utamaduni duniani.
Heshima hiyo inamfanya Kidjo kuwa mtu wa pili mzaliwa wa Afrika kuwahi kupata nyota katika barabara hiyo maarufu, baada ya mwigizaji wa Afrika Kusini Charlize Theron, aliyepokea nyota yake mwaka 2005.
Kidjo amejenga urithi wa kimataifa kwa kuchanganya mitindo ya muziki wa Kiafrika na Afrobeat, jazz na funk.
Zaidi ya muziki, ametumia jukwaa lake la kimataifa kuhamasisha uwakilishi wa Afrika, elimu, uwezeshaji wa wanawake na harakati za kijamii.