Maafisa wa polisi wamepata bunduki aina ya M16, inayoaminika kutekeleza mauaji manne tofauti katika kaunti ya Isiolo na kauti jirani ya Meru
Bunduki hiyo iliyokuwa na risasi 15, ilipatikana katika eneo la Kakili, baada ya operesheni ya kijasusi iliyotekelezwa na Huduma ya Taifa ya maafisa wa Akiba (NPRs) na Maafisa wa Serikali ya Taifa (NGAO).
“Kufuatia habari za kijasusi, kundi hilo lilipata bunduki aina ya M16 inayoaminika kumilikiwa na jangili Aloise Lochuchu almaarufu “Akoo,” ambaye hivi karibuni alishtakiwa kwa wizi wa kimabavu,” ilisema Huduma ya Taifa ya Polisi kupitia ukurasa wa X.
Baadhi ya mauaji yanayoaminika kutekelezwa na bunduki hiyo ni pamoja na mauaji katika eneo la Maili Tatu kaunti ya Meru mnamo Januari 26, 2025, mauaji ya mfanyabiashara katika kaunti ya Isiolo mnano Julai 20, 2025, mauaji katika eneo la Sakama, Isiolo mjini 24, 2025, na mauaji na naibu mkuu wa shule katika eneo la Leparua, kaunti ya Isiolo Kaskazini mnamo Februari 18, 2026.
” Upatikana kwa bunduki hiyo ni hatua kubwa kwenye uchunguzi wa mauaji hayo manne, na pia kubainisha iwapo imetumika katika mauaji mengine,” iliongeza huduma hiyo.
Bunduki hiyo kwa sasa inahifadhiwa katika kituo cha polisi cha Isiolo, kabla ikabidhiwe maabara ya uchunguzi wa kisayansi kwa uchunguzi zaidi.