Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu, haikuendelea leo Ijumaa, Agosti 14, 2026, kama ilivyokuwa imepangwa.
Hii ni baada ya shahidi wa 18 wa upande wa mashtaka kuripotiwa kupata dharura ya kiafya na kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe nyingine, ukieleza kuwa shahidi huyo alikuwa amepata tatizo la kiafya na kwenda hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo Lissu alipinga ombi hilo, akisema mahakama ilikuwa tayari imeelekeza upande wa mashtaka kuwasilisha angalau mashahidi wawili kila siku kesi hiyo inaposikilizwa, akiiomba mahakama ikatae ombi la upande wa mashtaka.
Lissu alisema alikuwa tayari kuendelea na kesi hiyo na kuutaka upande wa mashtaka kuwaleta mashahidi wengine mahakamani.
Alisema iwapo upande wa mashtaka hauna uwezo wa kuendelea kuwasilisha ushahidi, unapaswa kufunga kesi yake na kuruhusu suala hilo kuendelea katika hatua inayofuata, akidai kuwa upande wa mashtaka umeisha nguvu.
Hata hivyo, jopo la majaji watatu linalosikiliza kesi hiyo, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru na kusaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, lilikubali ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Agosti 17, 2026.