Rais William Ruto anahudhuria tamasha ya kitaifa ya mashindano ya muziki na densi kati ya taasisi mbalimbali za elimu nchini katika Ikulu Ndogo ya Bungoma.
Hii ni awamu ya 98 na kwa kawaida, huwa inahusisha maonyesho ya kazi za sanaa zilizoshinda katika kiwango cha kitaifa cha mashindano ya muziki na densi.

Tukio hilo ambalo ni kilele cha mashindano hayo ya muziki na densi kati ya taasisi za elimu, limewakutanisha maelfu ya wanafunzi wenye vipaji kutoka shule, vyuo na taasisi za elimu ya juu kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wanafunzi zaidi ya 143,000 wanashiriki tamasha ya mwaka huu, wakionyesha utajiri na utofauti wa Kenya katika muziki na sanaa zingine.

Rais Ruto ameandamana na Mama wa Taifa Rachel Ruto, Naibu Rais Kithure Kindiki, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba pamoja na viongozi wengine wakuu wa serikali.
Tamasha hiyo inatoa jukwaa la kusherehekea urithi wa kitamaduni wa Kenya na kukuza vipaji vya kisanii miongoni mwa vijana.
Pia inaangazia nafasi inayokua ya uchumi wa ubunifu na sanaa katika elimu, ukuzaji wa vipaji na maendeleo ya kitaifa.