Washukiwa sita wa ulanguzi wa binadamu wakamatwa Kiambu

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema sita hao walikamatwa katika nyumba moja ya vyumba viwili vya kulala katika eneo la Fort Jesus, Ruiru, kaunti ya Kiambu.

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa 6 wa ulanguzi wa binadamu wakamatwa Kiambu.

Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa sita wanaodaia kuhusika katika sakata ya ulanguzi wa binadamu, kaunti ya Kiambu.

Kwenye operesheni hiyo, maafisa hao pia waliwaokoa raia watatu wenye asili ya India ambao waliripotiwa kutoweka baada ya kuwasili nchini Kenya Agosti 5, 2026.

Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema sita hao walikamatwa katika nyumba moja ya vyumba viwili vya kulala katika eneo la Fort Jesus, Ruiru, kaunti ya Kiambu.

“Baada ya kushughulikiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), raia hao watatu waliingia kwenye teksi ambayo ilikuwa imekombolewa na mwenyeji wao, aliyekuwa akiwasubiri Ruiru,” ilisema DCI.

Baada ya kuwasili, walifungiwa kwenye nyumba hiyo bila ya kuwa na mawasiliano yoyote.

Waliokamatwa ni pamoja na Avtar Singh, raia wa India, Ali Khashif na Syed Shujaat Hussein, wote raia wa Pakistani, Stephen Karomo na Damaris Katulu Daudi, ambao ni raia wa Kenya.

Wakati huo huo raia wa Kenya mwenye umri mdogo anayedaiwa kuwa kijakazi pia alipatikana kwenye nyumba hiyo.

“Walipohojiwa, washukiwa hao walisema walikuwa wakiwasaidia raia hao wa India kusafiri kuelekea Italia kupitia Ethiopia,” iliongeza DCI.

Washukiwa hao wanazuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani.

TAGGED:
Share This Article