Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Igonga, amesema afisi yake iko tayari kukabiliana na kesi zinazohusiana na uchaguzi, huku taifa hili linapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027.
Akizungumza kwenye kongamano la viongozi Jijini Nairobi, Igonga alisema afisi yake imebuni kitengo maalum ambacho kimejukumiwa kushughulikia kesi za kiuchaguzi, kikipigwa jeki na viongozi wa mashtaka waliopokea mafunzo kuhakikisha kesi hizo zinashughulikiwa kwa wakati.
Igonga aliwaonya wale wanaolenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi kupitia ghasia, matamshi ya chuki, uhalifu wa mtandaoni, au uhalifu wa aina yoyote, kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema afisi yake itashirikiana kwa karibu na wadau wengine ikiwa ni pamoja na asasi za uchunguzi, uhakikisha Uchaguzi Mkuu mwaka 2027 unaandaliwa kwa mazingira ya amani, na wanaokiuka sheria za uchaguzi wanachukuliwa hatua.
Alidokeza kuwa sheria itatekelezwa kwa usawa bila ubaguzi, akisema maamuzi ya upande wa mashtaka hutekelezwa kwa njia huru kwa kuzingatia ushahidi uliopo.
Wengine waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na msemaji wa Huduma ya Taifa ya Polisi Muchiri Nyaga, mwenyekiti wa Tume ya Utangamano na Mshikamano wa Kitaifa Kasisi Kepha Omae, wanaharakati, wanafunzi wa Chuo kikuu cha Nairobi miongoni mwa wengine.