Serikali imetambua kaunti 18 ambazo ziko kwenye hatari ya kuathiriwa na mvua ya El Nino.
Huduma ya Utabiri wa Hali ya Hewa, tayari imedokeza kuwa taifa hili litapokea mvua ya kiwango cha juu, kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.
Kulingana na huduma hiyo, kuna uwezekano wa asilimia 81 kwamba mvua ya El Nino mwaka huu itakuwa kubwa, na uwezekano wa asilimia 97 kuwa athari zake zitadumu hadi mwaka ujao.
Na kama sehemu ya kukabiliana na athari za El Nino, serikali imetambua maeneo yako katika hatari ya kuathiriwa na mafuriko, maporomoko ya ardhi, ukame, kuzuka kwa magonjwa na uharibifu wa miundombinu.
Taasisi ya Kitaifa ya kuhusu Majanga (NDOC), imetaja maeneo ya Maziwa Makuu, Pwani, Bonde la Ufa na Kaskazini kuwa katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mvua hiyo.
Maeneo ya mijini ambayo yametajwa kuwa na hatari ya kuathiriwa na mvua hiyo ni pamoja na Nairobi, Mombasa na Kisumu.
Katika eneo la Pwani, maeneo ya Tana River, Kilifi, Lamu, Mombasa na Kwale huenda yakakumbwa na mafuriko, dhoruba na uharibifu wa miundombinu.
Eneo la Maziwa Makuu, Kisumu, Busia, Siaya, Homa Bay na Migori zinatarajiwa kukumbwa na mafuriko, maporomoko ya ardhi, kuzuka kwa magonjwa na visa vya watu kuachwa bila makazi.
katika eneo la Bonde la Ufa, Turkana, Baringo, Pokot Magharibi na Narok zitashuhudia ukame, mafuriko, maporomoko ya ardhi, kupoteza mifugo na ukosefu wa chakula.
Na katika kaunti za Garissa, Wajir na Mandera, kutakuwa na ukame, ukosefu wa maji, maafa ya mifugo, na ukosefu wa lishe ya mifugo na chakula cha binadamu.