Mahakama moja ya Kakamega imemhukumu mwanamume kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumdhulumu kimapenzi msichana wa umri wa miaka miwili.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Emily Owora, uliwaita maafisa wa kliniki kutoka hospitali ya kaunti ya Malava, ambao walithibitisha msichana huyo alidhulumiwa kingono.
Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Butali Reuben S. Kipngeno, alimhukumu kifungo hicho mwanamume huyo baada ya kupatikana na hatia hiyo, kuambatana na sehemu ya 8(1) pamoja na ile ya 8(2) ya sheria za kingono.
Mahakama ilifahamishwa kuwa kosa hilo lilitekelezwa Disemba 16, 2025, baada ya mama mtoto huyo kuondoka kidogo na kuwaacha mwanamume huyo na msichana kwenye chumba kimoja wakiwa wamelala.
Baadaye mama huyo aliona mtoto huyo akiwa na damu kwenye mkojo wake, ambapo alimpeleka hospitalini kwa matibabu. Baada ya uchunguzi wa kimatibabu alipatikana kuwa alidhulumiwa kingono.
Mtoto huyo alimtambua babake kama aliyemdhulumu kimapenzi.
Huku akijitetea, mwanamume huyo alidai kwamba alimwacha mtoto huyo peke yake nyumbani.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilibainisha kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa wa kuaminika, na kusababisha kuhukumiwa kwa mwanamume huyo.