Besigye aripotiwa kutoweza kuzungumza

Mkewe amesema mume wake anaona, anasikia, amekuwa akilala muda mrefu na bado hawezi kuzungumza wala kuandika kutohaka na udhaifu.

Marion Bosire
2 Min Read

Mke wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, Winnie Byanyima, ameelezea kwamba mume wake yuko katika hali hafifu hawezi kuzungumza.

Besigye wa umri wa miaka 70, ambaye ni mpinzani wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi jijini Kampala baada ya kuanguka mahakamani Julai 30, 2026.

Kesi inayomkabili ya uhaini ilikuwa ikiendelea siku hiyo wakati alianguka muda mfupi baada ya kupinga uamuzi wa mahakama wa kuteua mawakili wa kumwakilisha.

Wakili wake mkuu wa utetezi, Erik Lukwago, alikamatwa huku mwingine wa asili ya Kenya Martha Karua akizuiwa kuingia Uganda.

Byanyima amesema mume wake anaona, anasikia lakini ni mdhaifu sana na kwamba amekuwa akilala muda mrefu na bado hawezi kuzungumza wala kuandika kutokana na hali ya mikono yake kutokuwa imara.

Amesema awali Besigye alikuwa akipatiwa chakula kupitia mshipa wa damu, lakini baada ya hali yake kuimarika kidogo, mirija hiyo imeondolewa na ameanza kunywa supu.

Mwanasiasa huyo mkongwe wa Uganda alikamatwa nchini Kenya mwisho wa mwaka 2024 na kurejeshwa nchini Uganda ambapo baadaye alifikishwa mahakamani kwa madai ya uhaini.

Tangu wakati huo amesalia kizuizini huku Byanyima akiomba mamlaka nchini humo ziheshimi haki ya kuishi, kupata matibabu bora na kesi yake iendeshwe kwa njia ya haki.

Share This Article