Maafisa wa Polisi wamemkamata mshukiwa wa wizi wa simu katika eneo la likoni, kaunti ya Mombasa.
Mshukiwa huyo Prence Ndihokubwayo mwenye umri wa miaka 37 raia wa Burundi, alikamatwa baada ya maafisa wa polisi kutekeleza operesheni ya kijasusi kwenye duka lake katika eneo la Likoni.
“Baada ya kupokea habari za kijasusi, polisi walifanya msako kwenye duka la kuuza simu ambapo walipata simu 74 za mkononi kutoka kwa mshukiwa huyo,” ilisema Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kupitia ukurasa wa X.
Kulingana na DCI, simu hizo zinadaiwa kuwa ziliibwa kutoka kwa wananchi katika visa tofauti.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Likoni, akisubiri kufikishwa mahakamani.
Polisi wameanzisha uchunguzi kuwatafuta wenye simu hizo, huku wakijitahidi kubainisha ikiwa mshukiwa huyo ni sehemu ya mtandao mpana wa wahalifu unaohusika na wizi pamoja na ulanguzi wa simu zilizoibwa.