Sammy Douglas Waweru Kamau ameapishwa rasmi kuwa Mbunge mpya wa eneo la Ol Kalou, kufuatia ushindi wake katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika tarehe 16 Julai 2026.
Kamau aliapishwa baada ya kutia saini daftari rasmi la Kiapo cha Uongozi, katika hafla iliyoshuhudiwa na Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Mbunge wa Roysambu Augustine Kamande Mwafrika.
Kiti cha ubunge cha Ol Kalou kiliachwa wazi mwezi Machi 2026 kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge David Njuguna Kiaraho, aliyekuwa akihudumu muhula wake wa tatu baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kamau, aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha Democracy for Citizens Party, DCP, alishinda uchaguzi huo mdogo baada ya kupata kura 35,440 na kuwa mwakilishi mpya wa eneo hilo bungeni.
Mzaliwa huyo wa Ol Kalou ana shahada ya kwanza ya Uchumi wa Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. Alianza safari yake ya kisiasa mwaka 2013 baada ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi wadi wa kwanza wa Wadi ya Karau.
Kabla ya kuingia Bungeni, alihudumu kama mratibu wa DCP katika Kaunti ya Nyandarua, akiongoza shughuli za uhamasishaji wa chama mashinani.
Kamau atahudumu katika Bunge la 13 hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.