Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wawili, huku wakinasa bidhaa ghushi, kwenye operesheni ya kijasusi iliyotekelezwa katika eneo la Mwichio, kaunti ndogo ya Emuhaya, kaunti ya Vihiga.
Bidhaa hizo zinaaminika kumilikiwa na mshukiwa anayefahamika kwa jina la utani Moi, anayedaiwa kuhusika katika biashara ya bidhaa haramu, zikiwemo sigara na bidhaa za serikali za bei nafuu.
Wakati wa msako huo, polisi walipata masanduku 36 ya sigara aina ya Supermatch King Size, pamoja na masanduku mawili ya sigara aina ya Oris yanayopaswa kuuzwa kwa soko la nje ya nchi.
Wakati huohuo maafisa hao pia walinasa mifuko 50 ya kilo 50 kila moja ya mbolea ya gharama nafuu inayosambazwa na serikali kupitia Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB).
Washukiwa hao wawili Ruth Ongachi na Shem Amianda, wanazuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Uplelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilielezea kujitolea kukabiliana na biashara ya bidhaa ghushi kote nchini.
Wananchi wamehimizwa kutoa habari zitakazofanikisha kukamatwa kwa wale wanaohujumu uchumi wa taifa hili.