Saa chache baada ya Mahakama Kuu ya Milimani kumpata Gavana wa Zamani Okoth Obado na washtakiwa wenza wawili na hatia ya kumuua Sharon Otieno, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Igonga, amesema hiyo ni hatua kubwa katika upatikanaji wa haki.
Kupitia kwa taarifa, Igonga alielezea kurithishwa na uamuzi huo wa mahakama, akidokeza kuwa afisi yake inatarajia kuwa mahakama itatoa hukumu inayoashiria uzito wa kosa hilo.
“Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, amepongeza uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusiana na mauaji ya marehemu Sharon Otieno,” ilisema taarifa hiyo.
Huku akisema kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuwahusisha watatu hao na mauaji ya Sharon, Mkurugenzi huyo aliwapongeza viongozi wa mashataka wakiongozwa na Wangui Gichuhi ambaye ni Msaidizi Mkuu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (SADPP), Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), mashahidi na wadau wote wa mfumo wa upatikanaji haki ambao utaalam wao, na ushirikiano ulifanikisha uchunguzi na kuamuliwa kwa kesi hiyo.
Aidha, DPP alithibitisha kuwa afisi yake itaendelea kutafuta haki kwa usawa, bila uwoga, kwa utaalam na kuamabatana na katiba na mfumo wa sheria.
Justice Cecilia Githua alimpata Okoth Obado, msaidizi wake Michael Juma Oyamo na aliyekuwa karani wa kaunti ya Migori Casper Ojwang Obiero na hatia ya mauaji ya Sharon Otieno ambaye alikuwa mjamzito wakati wa mauaji hayo mwezi Septemba mwaka 2018.
Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 28, alikuwa mama wa watoto watatu alipotekwa nyara na kuuawa, tukio ambalo lilitausha taifa nzima.
Watatu hao sasa watazuiliwa hadi siku ambapo hukumu yao itatolewa, huku mahakama ikifutilia mbali dhamana zao.