Taasisi ya Utalii Kilifi kuanza kutoa mafunzo Septemba

Katibu wa Utalii, Julius Bitok, alitangaza maendeleo hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa chuo hicho.

Marion Bosire
2 Min Read

Chuo cha Ronald Ngala Utalii kilichoko Vipingo, Kaunti ya Kilifi, kitaanza rasmi kutoa mafunzo kwa kundi lake la kwanza la wanafunzi 1,000 mwezi Septemba.

Hatua inaweka historia ya kuanza kwa shughuli za taasisi hiyo ya kozi kuhusu ukarimu baada ya kusubiriwa kwa zaidi ya miaka 12.

Katibu wa Utalii, Julius Bitok, alitangaza maendeleo hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa chuo hicho akiwa ameandamana na Gavana wa Kilifi, Gideon Mung’aro na Mkuu na Afisa Mkuu Mtendaji wa Chuo cha Kenya Utalii, Mark Ogendi.

Alisema ujenzi wa chuo hicho umekamilika kwa asilimia 90 na kitakuwa tayari kupokea wanafunzi ndani ya siku 40 zijazo.

Bitok alieleza kuwa chuo hicho ni miongoni mwa taasisi bora zaidi barani Afrika kwa ubora wa miundombinu yake ya mafunzo ya ukarimu na utalii.

Alisema kitachangia pakubwa uzalishaji wa wataalamu wenye ujuzi watakaosaidia Kenya kufikia lengo la kuvutia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2030.

Katibu aliongeza kuwa taasisi hiyo itatoa kozi za ukarimu, usimamizi wa utalii, sanaa ya upishi, usimamizi wa safari na mafunzo ya kazi za meli za kitalii.

Gavana Mung’aro alisema kufunguliwa kwa chuo hicho kutaimarisha sekta ya utalii kwa kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi na kuongeza nafasi za ajira, hasa katika sekta inayokua kwa kasi ya meli za kitalii.

Mark Ogendi naye alisema chuo hicho kiko tayari kupokea wanafunzi wa ndani na wa kimataifa, akiongeza kuwa maombi ya kujiunga yanaendelea kupitia KUCCPS na Chuo cha Kenya Utalii.

Share This Article