Maafisa wa Polisi hususan Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI, wameimarisha uchunguzi kuhusu kifo cha Meneja wa Huduma za Sheria katika Huduma ya Misitu Kenya, KFS, Esther Wairimu Keige.
Mwili wa Keige ulipatikana katika shamba la kahawa huko Juja, Kaunti ya Kiambu, karibu mwezi mmoja baada ya kuripotiwa kutoweka.
Keige alitoweka Juni 10, 2026, baada ya dereva wake kumshusha katika kituo cha mafuta cha Shell mjini Juja, ambako alikuwa amepanga kupata taarifa kuhusu huduma za ukumbi wa mazoezi.
Kwa mujibu wa DCI, maafisa wa upelelezi walianzisha msako mkubwa uliojumuisha uchambuzi wa video za kamera za usalama, uchunguzi wa kitaalamu wa kisayansi, ukusanyaji wa taarifa za kijasusi, uchambuzi wa taarifa za simu ya mkononi na mahojiano na mashahidi.
Mwili wake uliokuwa umeanza kuoza ulipatikana Julai 6 ndani ya kibanda cha muda katika shamba la Fusion Estate Farm eneo huko Kiaora, Juja.
Polisi walipata simu yake ya mkononi ikiwa imezimwa katika eneo la tukio, huku viatu vyake vikiwa vimewekwa karibu na mwili. Baadaye, dadake alithibitisha utambuzi wa mwili huo.
Uchunguzi wa maiti haukubaini majeraha ya nje yanayoashiria shambulio na wataalamu wa uchunguzi wa maiti hawakuweza kubaini chanzo cha kifo kutokana na mwili kuwa katika hali ya kuoza sana.
Uchunguzi wa sumu mwilini na vipimo vingine vya kitaalamu unaendelea.
DCI imesema uchunguzi bado unaendelea na kusisitiza kuwa uwezekano wa mauaji bado haujaondolewa.
Maafisa wa upelelezi wamewataka wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kufafanua mazingira ya kifo cha Keige kujitokeza na kuzifikisha kwa polisi.