Walimu waliosahihisha mitihani ya KJSEA na KCSE 2025 walipwa

Walimu hao walinukuliwa wakitoa ilani ya kugoma kusimamia na kusahihisha mitihani ya mwaka huu ikiwa serikali ingekawia kuwalipa fedha hizo.

Martin Mwanje
1 Min Read
Julius Ogamba - Waziri wa Elimu

Walimu waliosimamia na kusahihisha Tathmini ya Kitaifa ya Wanafunzi wa Gredi ya Tisa nchini, KJSEA na Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka 2025 hatimaye wamelipwa salio la marupurupu yao. 

Hii ni takriban miezi minane baada ya walimu hao kukamilisha shughuli hiyo.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema fedha hizo tayari zimetumwa kwenye akaunti za walimu husika na Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini, KNEC.

“Ulipaji wa fedha hizo unafuatia kupokelewa kwa shilingi bilioni 1.5 kutoka kwa Hazina Kuu Julai 7, 2026, ukiwa ni mgao wa kugharimia salio hilo,” alisema Waziri Ogamba kwenye taarifa fupi leo Alhamisi.

“Tunawapongeza walimu waliosahihisha mitihani hiyo na wanataaluma wengine kwa utaalam wao, uvumilivu na dhamira endelevu ya kukuza ubora na uaminifu katika tathmini na mitihani yetu ya kitaifa.”

Awali, walimu hao walinukuliwa wakitoa ilani ya kugoma kusimamia mitihani ya mwaka huu ikiwa serikali ingekawia kuwalipa fedha hizo.

 

 

 

Share This Article