Mahakama Kuu itaanza kusikiliza kesi ya kupinga kung’atuliwa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua leo, vikao vitakavyoendelea kwa siku tatu mfululizo.
Gachagua aliwasilisha kesi hiyo mahakamani kupinga kuondolewa kwake mamlakani akisema hatua hiyo ilitekelezwa kinyume cha sheria.
Huku haya yakijiri, viongozi wa muungano wa upinzani ambao ni wandani wa Gachagua wamedhihirisha imani kwamba mahakama itamwondolea lawama.
Wakizungumza mjini Mombasa walikohudhuria ibada ya Jumapili, viongozi hao waliomba kikao cha majaji watatu wa mahakama kuu kilichojukumiwa kutatua kesi hiyo, kusikiliza mawasilisho vyema na kutoa uamuzi kwamba mchakato huo wa kumbandua ulikuwa na dosari tele.
Gachagua alisema, “Tuna imani katika mfumo wa haki nchini kwamba inafaa kuwa na uwezo wa kutoa haki kwa Rigathi Gachagua, wafuasi wake na watu wa Kenya.”
Eugine Wamalwa kwa upande wake alisema kwamba idara ya mahakama ndiyo suluhisho la mwisho la ulinzi na kwamba ndiyo taasisi iliyosalia pekee ambayo haijatekwa.
“Kuanzia keshi, uhuru huo wa idara ya mahakama, utawekwa kwenye mizani,” aliongeza kusema Wamalwa, viongozi wa pinzani wakihisi kwamba kesi hii itafichua jinsi sheria ilitumika kutatua ugomvi wa kibinafsi kati ya Gachagua na aliyekuwa mkubwa wake Rais William Ruto.
Kwa pamoja viongozi hao wanahisi kwamba kulikuwa na mwingilio na ushawishi katika bunge la taifa na bunge la Seneti kwa lengo la kuhakikisha mchakato wa kumbandua Gachagua unafuata mkondo fulani.