Jumla ya wachezaji 1,248 kutoka mataifa 48 watashiriki kipute cha Kombe la Dunia kati ya tarehe 11 mwezi huu na Julai 19 katika mataifa ya Mexico, Canada na Marekani.
Wanandinga 357 wanarejea kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya pili au zaidi, huku idadi iliyosalia ya wachezaji 891, wakitarajia kushiriki kwa mara ya kwanza.
Lionell Messi wa Argentina, Cristiano Ronaldo wa Ureno na kipa wa Mexico Guillermo Ochoa, watakuwa wakicheza Kombe la Dunia kwa mara ya sita kila mmoja.
Wachezaji 449 kutoka vilabu tofauti vya nchi 71 watashiriki fainali hizo huku Qatar na Saudi Arabia, zikiwa na idadi kubwa ya wachezaji wa ligi za nyumbani, wakiwa 25 kila moja.
Ivory Coast, DR Congo, Curaçao, Senegal na Uruguay, hazina mchezaji hata mmoja wa ligi ya nyumbani.
Wachezaji 22 wako chini ya umri wa miaka 20, huku wengine saba wakiwa zaidi ya umri wa miaka 40, na wengine 22 waliowahi kushinda Kombe hilo wakirejea kwenye fainali za mwaka huu.
Cape Verde, Curaçao, Jordan na Uzbekistan ndio mataifa manne yatakayoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Jumla ya mechi 104 zitachezwa katika viwanja 16 vilivyo katika miji 16 tofauti, katika nchi hizo tatu tofauti kuanzia Alhamisi ijayo.