Nchi za Afrika, hasa zile zilizo katika hatari ya kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, sasa zinatoa wito wa jitihada za pamoja katika kukabiliana na msambao wa ugonjwa huo.
Wito huo umetolewa wakati wa mkutano wa dharura wa makatibu wa afya zaidi ya 60 kutoka barani humo waliokutana kwa njia ya mtandao leo Jumatano asubuhi.
Mkutano huo, ambao pia uliwahusisha washirika wa maendeleo na mashirika ya kimataifa ya afya kutoka Afrika, uliongozwa na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni.
Kiini cha wasiwasi wao ilikuwa namna ya kusitisha ugonjwa huo hatari kabla ya kusambaa kwake katika nchi zingine za Afrika.
Wote hao wakikubaliana kwa kauli moja kuwa magonjwa huwa hayakosi kuvuka mipaka ya kitaifa na hivyo wanapaswa kufanya kazi bega kwa bega kudhibiti msambao wa ugonjwa huo.
Mlipuko wa aina ya virusi vya Bundibugyo vya ugonjwa wa Ebola katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda umekuwa tishio kwa mfumo dhaifu wa afya ya umma barani Afrika.
Nili iliyofanya washiriki kwenye mkutano huo, kwa karibu saa mbili, kuzungumzia mafanikio na mapungufu ya mifumo yao ya afya, na changamoto wanazokabiliana nazo katika kupiga dafrau msambao wa Ebola.
Changamoto zilizotajwa ni pamoja na ufuatiliaji usiotosheleza, mipaka ambayo ni rahisi kwa yeyote kuingia na kutoka, mifumo dhaifu ya uangalizi na rasilimali ndogo za tiba.
Licha ya changamoto hizo, viongozi hao walikubaliana juu ya hatua kadhaa za kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha uangalizi wa kuvuka mpaka na ufuatiliaji, pamoja na kufanya vipimo kwa pamoja katika maeneo ya kuingia katika nchi zao husika.