Wasanii nchini Uganda wamehimizwa watekeleze taratibu za kuwaweka kama nembo ili kuongeza ushawishi, badala ya kutegemea tu talanta.
Msanii wa kike wa nchi hiyo Nakiyingi Veronica Lugya almaarufu Vinka alikuwa akitoa maoni yake kuhusu kufanikiwa kama msanii anayesimamiwa na kampuni.
Alisisitiza kwamba talanta pekee haitoshi huku akimotisha wasanii kujemba nembo zao.
Msajiliwa huyo wa kampuni ya Swangz Avenue, anasema wasanii hawastahili kusubiri kampuni zinazowasimamia ziwafanyie kila kitu, bali wanafaa kuwajibika, iwapo wanataka mafanikio endelevu.
Akizungumza kwenye mahojiano kuhusu kuondoka kwa Zafaran kwenye Swangz Avenue, Vinka alieleza kuwa kampuni za muziki hujihusisha na hatari kubwa ya kifedha kila zinaposajili msanii mpya.
Alisema kuwa ingawa kampuni hizo huwekeza fedha nyingi katika vipaji vya wasanii, jukumu la kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo hubaki mikononi mwa msanii mwenyewe kwa kujenga chapa inayoweza kuuzika na kufanya kazi kwa bidii.
“Kuna mtu ameweka dau kwenye kipaji chako. Hajui kama fedha zake zitarudi au la. Atawekeza, lakini mwisho wa yote kila kitu kinategemea wewe,” Alisema akiongeza kwamba chapa ni muhimu katika mtazamo wa mashabiki na mauzo.
Vinka pia alipuuza dhana iliyozoeleka kwamba kusajiliwa na kampuni ya muziki kunahakikisha mafanikio moja kwa moja.
Kulingana naye, msanii anaweza kupata watunzi wa nyimbo wa kitaalamu, msaada wa kifedha, mavazi na rasilimali nyingine, lakini mambo hayo pekee hayawezi kumfanya kuwa nyota.
Alisisitiza kuwa ari binafsi, uthabiti na kujenga chapa ndiyo mambo yanayowatofautisha wasanii wanaofanikiwa na wengine.
Aidha, Vinka aliwasihi wanamuziki wanaotarajia kusajiliwa na kampuni za muziki kuelewa uhalisia wa maisha ndani ya kampuni hizo kabla ya kusaini mikataba.