Polisi waimarisha vita dhidi ya mihadarati, washukiwa 5 wakamatwa

Watano hao walikamatwa baada ya maafisa hao kutekeleza operesheni Mombasa, Kitengela na Busia.

Tom Mathinji
2 Min Read
Polisi waimarisha vita dhidi ya ulanguzi wa mihadarato kote nchini.

Maafisa wa kitengo cha kukabiliana na mihadarati (ANU), wamewakamata washukiwa watano wanaodaiwa kuhusika na ulanguzi wa mihadarati hapa nchini.

Watano hao walikamatwa baada ya maafisa hao kutekeleza operesheni Mombasa, Kitengela na Busia.

Katika kaunti ya Mombasa, maafisa hao walisimamisha lorry lenye nambari za usajili KDL 220P, na baada ya kulipekua walipata magunia 9 ya bangi yenye uzani wa kilo 450, ya thamani ya shilingi 12,150,000. Dereva wa lori hilo Emmanuel Ndoro, na mshirika wake Paul Ogolla, walikamatwa papo hapo.

Katika eneo la Kitengela, Makachero walitekeleza operesheni kwenye kituo cha kibiashara cha Honey Pot Bar, ambapo walipata marobota mawili ya bangi, mfuko wa plastiki ambao pia unaaminika kuwa na bangi, huku mshukiwa Catherine Nzuki, alitiwa nguvuni.

Na katika kaunti ya Busia, maafisa wa polisi walifanya msako katika eneo la Butula Mission, ambako walisimamisha gari lenye nambari za usajili KBR 254P, na baada ya kulipekua walipata magunia mawili ya bangi.

Waliokuwa kwenye gari hilo Ibrahim Oduor Otieno na Alma Nzimi Muiya, walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Busia.

Washukiwa hao watano wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Kwenye ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema msako utaendelea kwa lengo la kutokomeza ulanguzi wa mihadarati kote nchini.

TAGGED:
Share This Article