Halmashauri ya Taifa ya Usimamizi wa Barabara Kuu nchini (KeNHA), imetangaza kufungwa kwa muda kwa sehemu ya barabara ya Waiyaki Way jijini Nairobi.
Kulingana na KeNHA, sehemu ya barabara hiyo itafungwa kwa muda wa miezi mitatu, ili kufanikisha ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya watembezi katika eneo la Westlands.
Sehemu itakayoathiriwa ni eneo la Karuna Close na mzunguko wa magari wa Westlands, na itafungwa kwa muda kuanzia tarehe 25, mwezi Juni hadi tarehe 25, mwezi Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa ilani iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri ya KeNHA mhandisi Luka Kimeli, hatua hiyo itatoa fursa ya upanuzi wa kivuko cha watembeaji miguu katika eneo la Dunhill Towers pamoja na ujenzi wa kivuko kipya cha watembeaji katika mzunguko wa Westlands.
Wakati wa shughuli za ujenzi, usafiri utaelekezwa kupitia safu ya barabara jinsi ilivyobainishwa katika mpango wa usimamizi wa shughuli za uchukuzi.
Aidha, kwenye ilani hiyo madereva wameshauriwa wawe waangalifu na kufuata kanuni zote za trafiki katika maeneo yaliyoathirika.