Viongozi wa Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani, G7 wameelezea kujitolea kwao kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda, huku pia wakielekezea juhudi zao kupiga vita saratani kote duniani.
Hayo yalitangazwa wakati wa mkutano wa G7 ulioandaliwa jijini Evian nchini Ufaransa.
Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi kutoka mataifa wanachama wa G7 ambayo ni Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza na Japani.
Viongozi wengine walioalikwa mkutanoni kutoka Kenya, Brazil, Misri, India na Korea Kusini pia walishiriki.
Kwenye tangazo la pamoja, viongozi hao walisema chamko la ugonjwa wa Ebola nchini DRC na Uganda, linaashiria hatari ya usalama wa afya, huku wakitoa wito wa ushirikiano wa pamoja kukabiliana na maambukizi zaidi.
Walielezea wasiwasi kutokana na maafa na athari katika jamii zilizoathiriwa, wakidokeza kuwa juhudi za kutokomeza ugonjwa huo zimedumazwa na mzozo unaoendelea katika eneo hilo.
Aidha, walielezea kujitolea kwao kufanikisha juhudi za kupata na kuwasilisha chanjo na upatikanaji wa matibabu ili kusitisha chamko hilo.
Wakati huo huo, viongozi hao wa chumi zilizostawi zaidi duniani pia walielezea umuhimu wa kukabiliana na ugonjwa wa saratani, wakionya kuwa unasalia kuwa changamoto kuu ya kiafya.
Walidokeza kuwa saratani husababisha vifo vya watu milioni kumi duniani kila mwaka, wakisema maambukizi mapya yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 80 kufikia mwaka 2050 kutokana na masuala ya kimazingira.
Viongozi hao wa G7, walielezea kujitolea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu utafiti wa saratani ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa takwimu za saratani kwa watoto na vijana, wakipigia debe utumiaji wa akili unde na teknolojia ya kidijitali katika kutambua na kutibu ugonjwa huo.
Rais wa Kenya William Ruto ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano huo wa G7, kwa mwaliko wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.