Wizara ya Elimu imevuna pakubwa katika bajeti ya mwaka 2026/2027, ikitengewa shilingi bilioni 784.5, hii ikiwa sawia na asilimia 26.8 ya bajeti yote.
Kwenye mgao huo, Tume ya kuwaajiri Walimu (TSC), imetengewa shilingi bilioni 424.3, nayo idara ya Elimu ya Msingi ikipokea shilingi bilioni 136.6.
Akiwasilisha bajeti ya mwaka 2026/2027 kwenye Makengo ya Bunge siku ya Alhamisi, Waziri wa Fedha John Mbadi, alipendekeza shilingi 163.9 zitumiwe katika idara ya Elimu ya juu, shilingi bilioni 1.3 kwa uvumbuzi wa sayansi na utafiti, huku Taasisi za Elimu ya kiufundi zikipokea shilingi bilioni 58.5.
Aidha, elimu ya msingi bila malipo imetengewa shilingi bilioni 7, huku elimu ya sekondari msingi ikipokea shilingi biliono 30.7 Usimamizi wa mitihani ya kitaifa utapokea shilingi bilioni 9.9, na mpango wa lishe shuleni ukitengewa shilingi bilioni 3.
Shilingi biliono 4.9 zitatumika kuwaajiri walimu wanagenzi 20,000 kwa ajira ya kudumu, na shilingi bilioni 8.2 za kuwaajiri walimu wapya wanagenzi ili kupunguza nakisi ya walimu iliyopo ili kumarisha matokeo ya elimu.
Wakati huo huo, Mbadi amependekeza shilingi bilioni 2.1 zitumike katika ujenzi na kuweka vifaa kwa taasisi za TVET, na shilingi bilioni 56.3 kwa Bodi ya kutoa Mikopo kwa elimu ya vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi.