Waziri wa Fedha John Mbadi ametangaza kuwa sekta ya Afya itapokea mgao wa shilingi bilioni 177.2, kwenye bajeti ya mwaka 2026/2027.
Akitangaza hayo leo Alhamisi alipokuwa akisoma bajeti hiyo kwenye Majengo ya Bunge, Mbadi alisema mgao huo unalenga kuimarisha Huduma za Afya kwa Wote (UHC), pamoja na kuboresha huduma zingine muhimu za afya kote nchini Kenya.
Kulingana na Mbadi, kati ya mgao huo wa shilingi bilioni 177.2, shilingi bilioni 8.2 zitatumika kulipa mishahara ya wafanyakazi wanaotekeleza mpango wa UHC, shilingi bilioni 19.1 zitumike kwa hazina ya afya ya msingi kufadhili huduma za mstari wa mbele, huku shilingi bilioni 18.5 zikitengwa kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza.
Wakati huo huo Mbadi alipendekeza shilingi bilioni 6.4 zitumiwe kwa mpango wa utengenezaji dawa na utoaji wa chanjo, kwa lengo la kuwakinga watoto na jamii dhidi ya changamoto za kiafya nchini Kenya.
Aidha, Mbadi alieleza kuwa vita dhidi ya ugonjwa wa saratani vinahitaji uwekezaji zaidi, huku akipendekeza shilingi bilioni tatu kwa hazina ya dharura, ili kukabiliana na saratani na magonjwa mengine sugu. Shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ujenzi wa kituo cha kutibu saratani katika hospitali ya Kisii Level 5, huku akipendekeza shilingi milioni 300 zitumiwe kuimarisha matibabu ya saratani katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta, na shilingi milioni 150 kwa upanuzi wa kituo cha saratani katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Mafunzo na Rufaa ya Kenyatta.
Hospitali za rufaa kote nchini pia hazijaachwa nyuma, kwani kwenye bajeti hiyo zimetengewa shilingi bilioni 45.3, huku halmashauri ya kusambaza vifaa vya matibabu nchini (KEMSA), ikitengewa shilingi bilioni 20.9 ili kuimarisha huduma zake, nayo Taasisi ya Utafiti wa Matibabu (KEMRI) ikipokea shilingi bilioni 3.1.
Wanagenzi wa kimatibabu wametengewa shilingi bilioni 9.3 ili kuimarisha utendakazi katika sekta ya afya, huku Taasisi ya Mafunzo ya Utabibu KMTC, ikipokea shilingi biloni 10.9 na maafisa wa afya ya jamii wakitengewa shilingi bilioni 3.2.
Sekta hiyo ya afya imepokea mgao huo, wakati ambapo kanda hii inakabiliwa na tisho la ugonjwa wa Ebola ambao umezuka katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC).