Waziri wa Afya Aden Duale, amesema Kenya imeimarisha juhudi zake za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, kuoitia utoaji mafunzo kwa maafisa wa afya.
Kulingana na Duale, mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa taifa hili wa kugundua, kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utazuka.
Akizungumza Jumatano alipofungua warsha ya kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya siku nne Jijini Nairobi, Duale alisisitiza kwamba kuwa tayari ni nguzo kuu katika usalama wa afya, akidokeza kuwa Kenya iko kwenye hatari ya kuambukizwa kutokana na hali ya kuwa kitovu cha usafiri na biashara katika kanda hii.
Alisema kuwa mafunzo hayo yatapiga jeki ubadilishanaji wa maarifa na ufahamu kwa kaunti na kaunti ndogo, ili kuimarisha utayari wake kwa dharura za afya ya umma.
Duale alidokeza kuwa mlipuko wa magonjwa kwenye kanda hii, umeashiria umuhumu wa kuwa na mifumo dhabiti ya kuzuia na kudhibiti magonjwa katika vituo vya afya.
Aliwapongeza wahudumu wa afya nchini Kenya kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, akisema wahudumu hao ndio uti wa mgongo wa juhudi za kukabilina na magonjwa.
Aidha, aliwasihi Wakenya kuwa na imani na juhudi za serikali za kukabiliana na Ebola, ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa kituo cha Karantini.
Watu zaidi ya 300 wamefariki kutokana na makali ya Ebola katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), huku juhudi za pamoja za kimataifa zikitekelezwa kusitisha msambao wake.