Viongozi wa Laikipia wapinga pendekeo la ujenzi wa Karantini

Tom Mathinji
2 Min Read
Maafisa wakikabiliana na ugonjwa wa Ebola / Picha ya awali kwa hisani ya IFRC

Viongozi wa kaunti ya Laikipia wamepinga vikali pendekezo la ujenzi wa kituo cha karantini cha wagonjwa wa Ebola mjini Nanyuki.

Wakiongozwa na Gavana wa Laikipia Joshua Irungu, viongozi hao walikataa pendekezo hilo linaloungwa mkono na  marekani la kujenga kituo cha karantini na matibabu kwa wagonjwa wa   Ebola katika kituo cha jeshi la wanaanga cha Laikipia.

Akiwahutubia wakazi  gavana Irungu alizungumzia hatari za kiafya kwa wakazi.  Irungu aliwahakikishai wakazi kwamba viongozi wa eneo hilo watailinda jamii na kuwahimiza kuwa watulivu.

Kwa upande wake Seneta wa Laikipia John Kinyua, aliinyoshea kidole cha lawama serikali ya Kenya kwa kile alichokitaja kimeshindwa kuzingatia usalama wa wakenya kupitia mpango huo.

“Tunakataa pendekezo hilo. Mbona ambao wanaugua ugonjwa huo wasipelekwe katika nchi zao ikiwa Ebola sio ugonjwa hatari,?” aliuliza Kinyua.

Mwakilishi wa wadi ya Igwamiti, Irene Wacuka na mzee John Mundia, walikariri kuwa usalama na maslahi ya wakazi wa Laikipia ni sharti upewe kipaumbele.

Walisema kuwa hawataki kituo hicho kijengwe katika eneo hilo, wakiibua hofu kwmaba chamko la ugonjwa huenda likasababisha vifo vya wakazi.

Viongozi hao sasa wanatoa wito kwa serikali kutathmini mpango huo na kuwahusisha wakazi wa eneo hilo kabla ya kufanya maamuzi kuhusu pendekezo hilo.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Kenya imesitisha kwa muda pendekezo la serikali ya Marekani la kufungua kituo cha karantini nchini Kenya, kitakachotumiwa kuwatenga raia wake watakaobainika kuambukizwa ugonjwa wa Ebola.

Mahakama ilichukua hatua hiyo baada ya Taassisi ya Katiba Kenya kuwasilisha kesi kwenye mahakama hiyo kupinga pendekezo hilo la Marekani.

Share This Article