Waziri wa Elimu Julius Ogamba, ametangaza kuvunjwa kwa Bodi ya Usimamizi wa Utumishi Girls Academy, kufuatia mkasa wa moto siku ya Alhamisi.
Kwenye mkasa huo wanafunzi 16 walifariki, huku zaidi ya 70 wakijeruhiwa na wanaendelea kupokea matibabu.
Kupitia kwa taarifa leo Ijumaa, waziri huyo alishtumu usimamizi wa shule hiyo kwa kukosa kuzingatia miongozo ya kiusalama ya shule hiyo na ile ya Idara ya Elimu ya Msingi.
“Kulikuwa na msongamano wa wanafunzi na mlango mmoja wa bweni hilo ulikuwa umefungwa kinyume na mikakati ya kiusalama iliyowekwa,” alisema Waziri Ogamba.
Huku akitaja mkasa huo kuwa wa kupangwa, waziri huyo alisema walimu wawili walifahamishwa kuhusu mpango wa kuteketeza shule hiyo, lakini walipuuza habari hizo na kukosa kuchukua hatua zozote.
“Walimu ambao walifahamishwa kuhusu njama hiyo lakini wakakosa kuchukua hatua, pia watachukuliwa hatua za kinidhamu,” aliongeza waziri huyo.
Wakati huo huo, Ogamba alisema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo atachukuliwa hatua kwa kukosa kuzingatia miongozi ya kiusalama ya shule hiyo na ile ya Idara ya Elimu ya Msingi.
“Uchunguzi unaendelea kubaini ikiwa kulikuwa na utepetevu kwa maafisa wa elimu na wale wa Tume ya kuwaajiri Walimu. Hatua zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote atakayepatikana na hatia ya kuzembea kazini,” alidokeza Ogamba.
Wanafunzi wanane tayari wanazuiliwa na polisi kwa madai walihusika katika mkasa huo wa kutamausha.