Katibu katika wizara ya Afya Mary Muthoni, amesema Kenya imepiga hatua kubwa kuwa kitovu cha huduma bora za afya katika kanda hii.
Alisema hayo yanafanikishwa na kuimarishwa kwa huduma za afya za msingi hadi utoaji huduma za afya kwa njia za dijitali.
Akizungumza katika kongamano la Nation Health Summit 2026 Jijini Nairobi, Muthoni alielezea mageuzi ambayo yametekelezwa katika sekta ya afya ambazo ni pamoja na kuwaajiri maafisa wa jamii wa afya 107,000, upanuzi wa huduma maalum za matibabu na uwekezaji katika utengenezaji wa dawa hapa nchini.
Katibu huyo alidokeza kuwa kanda ya Afrika Mashariki, inauwezo wa kuwa na huduma bora za afya, utafiti wa kimatibabu na ukuaji wa nguvukazi kupitia ushirikiano wa kimkakati, teknolojia na mifumo bora ya afya.
Kongamano hilo limewaleta pamoja viongozi katika sekta ya afya, watungaji sera, wabunifu, wawekezaji na wadau kutoka katika kanda hii.