Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, amepuuzilia mbali madai kwamba serikali inalenga kuiba kura kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, akisema kuwa utawala wa Kenya Kwanza utachaguliwa tena kutokana na rekodi bora ya miradi ya maendeleo.
Akizungumza Jumatatu katika kaunti ya Kisii, kindiki alisema serikali haina sababu yoyote ya kuvuruga mchakato wa uchaguzi, kwa sababu utendakazi wake tayari unaungwa mkono na wananchi kote nchini.
“Hatuhitaji usaidizi haramu kushinda Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema Kindiki.
Prof Kindiki alidokeza kuwa utawala wa Rais William Ruto umewekeza pakubwa katika sekta ya barabara, uunganishaji wa umeme, nyumba za bei nafuu, kilimo, afya na mabadiliko katika sekta ya elimu, maendeleo ambayo yatawachochea Wakenya kuipigia kura serikali.
Aidha, Naibu huyo wa Rais alikosoa upande wa upinzani kwa kuendesha siasa za mapema alizotaja zinaongozwa na propaganda, badala ya kutoa suluhu kwa changamoto zinazowakabili Wakenya.
“Mwaka ujao wakenya watachagua kati ya maendeleo na dhana potovu,” aliongeza Kindiki.
Huku akishikilia kuwa serikali haina lengo la kuvuruga mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, Kindiki alionya kuwa matanshi kama hayo yanaweza kusababisha taharuki na kupoteza imani katika taasisi za kidemokrasia nchini Kenya.