Washukiwa wa wizi wanaswa na mali kupatikana

Walikamatwa katika misako iliyotekelezwa na maafisa wa upelelezi na maafisa wa polisi katika sehemu mbali mbali za nchi.

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa upelelezi wa jinai nchini DCI wametangaza kukamatwa kwa washukiwa wa wizi uliofanyika wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025 katika soko la Kiritiri, eneo bunge la Mbeere Kusini kaunti ya Meru.

Wakishirikiana na maafisa wa polisi wa kituo cha polisi wa Kiritiri, maafisa hao waliwakamata Francisca Mwingi na Linda Karimi na kupata tangi la maji la rangi nyeupe, mojawapo ya bidhaa nyingi zilizoibwa kutoka soko la Kiritiri siku hiyo.

Katika misako mingine ya maafisa wa usalama katika maeneo ya Kikuyu na Dagoretti gari la uchukuzi wa umma aina ya Nissan nambari ya usajili KAW 702K lilinaswa.

Gari hilo linaaminika kutumika kusafirisha waharibifu kutoka eneo la Gachui-Mutuini hadi Dagoretti ambapo waliiba bunduki, sare za polisi, wakashambulia maafisa wa polisi na kuchoma kituo cha polisi.

Washukiwa wanne, Sammy Ndungu Kariuki almaarufu Ndoji, Lawrence Kariuki Ndungu, Ali Shama Tabet almaarufu Alibaba na Simon Njoroge Hiuhu walikamatwa baada ya kupatikana na mali iliyoibwa Jumatano wakati wa maandamano.

Katika eneo la Maai Mahiu kaunti ndogo ya Naivasha kaunti ya Nakuru, washukiwa saba walitiwa mbaroni huku maafisa wakinasa mali iliyokuwa imeibwa.

Washukiwa hao wote wanaandaliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani ambapo watakabiliwa na mashtaka mbali mbali kama vile uharibifu wa mali na uchomaji.

Website |  + posts
Share This Article