Watu 11 wafariki katika maporomoko ya mgodi wa dhahabu Sudan

Mgodi husika ulikuwa umetangazwa awali kuwa hatari lakini shughuli zikaendelezwa huko.

Marion Bosire
2 Min Read

Watu 11 wamethibitishwa kufariki kufuatia kuporomoka kwa sehemu ya mgodi wa dhahabu katika eneo la Kaskazini Mashariki la Sudan ambapo wengine saba walijeruhiwa.

Haya ni kulingana na kampuni ya serikali ya uchimbaji madini, tukio linalojiri wakati ambapo makabiliano kati ya jeshi la serikali ya Sudan na kundi la RSF yanaendelea kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Pande zote za makabiliano hayo zinadaiwa kufadhiliwa na pesa zinazotokana na biashara ya dhahabu.

Katika taarifa Jumapili, kampuni ya Sudanese Mineral Resources -SMRC ilielezea kwamba mgodi ulioathirika ni wa Kirsh al-Fil ambao uko katika eneo la mashinani la jangwa la Howeid.

SMRC ilifafanua kwamba ilikuwa imesimamisha shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huo na kutoa onyo kwa wahusika kwamba ulikuwa hatari.

Sudan ambayo ndiyo nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika, ni moja kati ya nchi zinazozalisha kiwango kikubwa cha dhahabu barani humu, nyingi ikitokana na wachimbaji madini wa kiwango cha chini.

Tofauti na kampuni zilizo na vifaa na mashine za kufanikisha uchimbaji huo, wachimbaji wa migodi midogo hawana vifaa vya kujilinda na mara nyingi hutumia kemikali zinazosababisha maradhi.

Maporomoko ya migodi hushuhudiwa mara kwa mara nchini Sudan likiwemo poromoko la mwaka 2023 ambapo watu 14 walipoteza maisha na jingine la mwaka 2021 ambapo watu 38 waliaga dunia.

Website |  + posts
Share This Article