Viongozi kutoka Magharibi mwa nchi wameanza kujipigia debe wakimtaka Rais William Ruto kumteua Naibu Rais kutoka eneo hilo katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.
Wakizungumza na wanahabari katika hoteli moja mjini Naivasha jana Jumapili, viongozi hao waliojumuisha Magavana, Maseneta na Wabunge 28, walisema eneo la Magharibi lina idadi kubwa ya wapiga kura, hivyo basi linapaswa kutoa mgombeaji mwenza wa Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Aidha, walikariri kumuuunga mkono Rais Ruto kwa hali na mali kuchaguliwa kwa muhula pili.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na magavana wa kaunti za Magharibi.
Kwa kauli moja, waliitaka jamii ya Waluhya kuwa na sauti moja kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Wito wao unakuja wakati ambapo viongozi kutoka maeneo ya Nyanza na Pwani wamekuwa pia wakivizia kiti hicho ambacho kwa sasa kinashikiliwa na Prof. Kithure Kindiki.
Viongozi kutoka Mlima Kenya wameapa kuhakikisha kiti hicho kinasalia eneo hilo wakati wa uchaguzi mkuu ujao.