Rais William Ruto amewasili Afrika Kusini kwa ziara rasmi ya siku mbili, kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa.
Akiwa ameandamana na Mama Taifa Rachel Ruto, kiongozi wa taifa alitua katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Waterkloof Airforce jijini Pretoria, na kulakiwa na Naibu Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano Alvin Botes.
Juma lililopita, Rais Ramaphosa kupitia ukurasa wake wa X, alisema amemwalika kiongozi huyo wa Kenya kufanya ziara nchini humo kuanzia Juni 3 hadi Juni 5, 2026.
“Rais Ruto atafanya ziara ya kiserikali kuanzia Juni 3 hadi 5 kwa mwaliko wa Rais Ramaphosa. Afrika Kusini inadhamini Kenya kama mshirika wa kimkakati katika kanda ya Afrika Mashariki na katika bara hili,” alisema Ramaphosa alipokuwa akitoa ratiba ya ziara hiyo.

Afrika Kusini na Kenya zimefurahia ushirikiano wa muda mrefu ambao ni wa manufaa kwa pande mbili tangu uhusiano wa kidiplomasia kubuniwa upya mwaka 1994.
Kulingana na Ramaphosa, ziara hiyo rasmi itajumuisha sherehe ya makaribisho, na kufuatiwa na mazungumzo ya pande mbili kati ya viongozi hao wawili na kisha mkutano wa kibiashara utakaowajumuisha maafisa wa serikali na wale wa sekta ya kibinafsi kutoka nchi hizo mbili.
Mkutano huo wa kibiashara utalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kubuni mikakati ya kupanua fursa za kibiashara na uwekezaji katika sekta muhimu kwa manufaa ya nchi hizo mbili.