Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia,timu nne bora kwenye msimamo wa FIFA, zimejikatia tiketi kushiriki nusu fainali itakayopigwa baina ya Jumanne na Jumatano hii.
Ufaransa inayoorodheshwa ya kwanza duniani itakabiliana na Uhispania iliyo ya tatu kwenye nusu fainali ya kwanza Jumanne, Julai 14, katika uwanja wa Dallas,nchini Marekani ,kuanzia saa nne usiku.
Timu zote mbili pia zinajivunia kutopoteza mechi katika kipute cha mwaka huu,Ufaransa wakiwa na asilimia 100 ya ushindi nao Uhispania wametoka sare moja pekee.
Mabingwa watetezi Argentina wanaokalia nafasi ya 2 duniani kwenye msimamo wa FIFA,watapimana ubabe na Uingereza inayoshikilia nafasi ya nne,katika nusu fainali ya pili siku ya Jumatano, Julai 15.
Argentina pia hawajapoteza mechi sawia na Uingereza katika makala ya mwaka huu.
Washindi wa nusu fainali watakabiliana kwenye fainali Jumapili hii mjini New York ,huku washinde wakikwangurana Jumamosi mjini Miami, katika mechi ya kuwania nishani ya shaba.
Jumla ya mabao 292 yamefungwa katika michuano 100 ya patashika hiyo,ikiwa wastani wa magoli 2.92, katika kila mechi.
Lionel Messi wa Argentina na Kylian Mbappe wa Ufaransa,wangali wafungaji bora kwa mabao 8 kila mmoja,moja zaidi ya Erling Braut Halaand wa Norway, wakati Harry Kane na Jude Bellingham wa Uingereza, wakiwa wamepachika magoli 6 kila mmoja.
Kila timu iliyobanduliwa katika robo fainali itatuzwa dola milioni 19 sawa na shilingi bilioni 2.4 kila moja,zikiwa Morocco,Uswizi,Norway na Ubelgiji.