Kampeni Ol Kalou kumalizika leo kabla ya uchaguzi Alhamisi

Sheria inahitaji kampeni kusitishwa saa 48 kabla ya kura kupigwa, na wagombea wana hadi saa kumi na mbili leo jioni kuhitimisha kampeni zao.

Martin Mwanje
1 Min Read

Wagombea katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou wana muda wa chini ya saa tisa kuwashawishi wapiga kura kuwaunga mkono katika uchaguzi mdogo utakaoandaliwa Alhamisi wiki hii. 

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasema kampeni zitamalizika saa kumi na mbili jioni leo Jumatatu.

Sheria inahitaji kampeni kusitishwa saa 48 kabla ya kura kupigwa.

Wagombea wanazuru kila pembe ya eneo bunge hilo kabla ya wapiga kura kuamua nani atakayekuwa mbunge wao mpya.

Ushindani mkali umeibuka hasa kati ya mgombea wa chama tawala cha UDA Muchina Nyagah na Sammy Ngotho wa chama cha DCP chake Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.

Hata hivyo, kumekuwa na madai ya kuwahonga wapiga kura na visa vya vurugu vilivyoshuhudiwa katika eneo hilo huku magari ya kampeni ya upinzani yakilengwa.

Wakati mmoja, IEBC ilitishia kuahirisha uchaguzi huo ikiwa itabaini mazingira ya kuuandaa si salama.

Ni tishio lililopingwa vikali na upande wa serikali na ule wa upinzani.

Uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Ol Kalou unaandaliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

 

Share This Article