Wakenya wahimizwa kujiepusha na siasa za migawanyiko

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto afungua soko la samaki la Malindi.

Rais William Ruto amepuuzilia mbali siasa ambazo zinawagawanya wananchi na alizosema zimedumaza miradi ya maendeleo  katika sehemu kadhaa za nchi, eneo la Pwani likiwemo.

Akizungumza Ijumaa katika kaunti ya Kilifi, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa utawala wake unajibiisha kuwaunganisha Wakenya kutoka miegemeo tofauti ya kisiasa, ili kupiga kumbo ukabila, siasa potovu na ubaguzi.

Aliyasema hayo alipofungua soko la samaki la Malindi na kukabidhi mashua kwa makundi ya wanawake na vijana ili kuimarisha sekta ya uvuvi na kuimarisha maisha.

Rais aliongeza kuwa serikali imewekeza shilingi bilioni 2.7 katika ujenzi wa barabara katika kaunti ya Kilifi, ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi na kijamii.

“Tumewekeza pia shilingi bilioni 12 kwa upanuzi wa uunganishaji umeme, usambazaji na udhabiti katika kaunti ya Kilifi,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto yuko kwenye ziara rasmi ya kimaendeleo katika eneo la Pwani.

Share This Article