Uganda yafutilia mbali hofu ya ebola, yasema iko salama

Martin Mwanje
1 Min Read

Nchi jirani ya Uganda imefutilia mbali hofu ya kuenea kwa ugonjwa wa ebola nchini humo ikisema iko salama kutembelewa wakati wowote. 

Kwenye taairifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Utalii ya nchi hiyo (UTB) Juliana Kagwa amesema licha ya visa viwili vya ugonjwa huo kuripotiwa nchini humo, hakuna haja ya kuhofu.

“Uganda imeripoti visa viwili kutoka nje ya nchi hiyo vinavyohusisha raia wa Congo walioingia Uganda kutokea DRC. Kwa bahati mbaya, mgonjwa mmoja alifariki na amerejeshwa nchini mwake, huku wa pili akiendelea kutibiwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Afya,” alisema Kagwa.

“Muhimu zaidi, kuna maambukizi SIFURI kwa sasa ndani ya nchi au maambukizi katika jamii ndani ya Uganda. Wizara ya Afya ya Uganda inaendelea kufanya uangalizi mkali, kufanya vipimo, ufuatiliaji, na uitikiaji wa haraka nchini kote.”

Afisa huyo amesema Uganda ina tajiriba ya kudhibiti milipuko ya ugonjwa wa ebola na magonjwa mengine ya milipuko, na kwa misingi hiyo, shughuli zingine kama vile utalii na huduma za usafiri zinaendelea kama kawaida.

Watalii na wadau wa utalii wametakiwa kuzingatia viwango vya juu vya usafi ikiwa ni pamoja na kunawa mikono wakati wakiwa nchini humo.

 

Share This Article