Rais Ruto amuomboleza Anita Kendi Murungi

Tom Mathinji
1 Min Read
Anita Kendi Murungi.

Rais William Ruto amewaongoza viongozi wengine nchini Kenya, kuomboleza na familia ya Gavana wa zamani wa Meru Kiraitu Murungi, kufuatia kifo cha binti yake Anita Kendi Murungi. 

Kwenye ukurasa wake wa X, kiongozi wa nchi alisema ni huzuni kubwa kumpoteza mtoto hasaa mwenye umri mdogo, mwerevu na aliyejawa na matumaini sio haba.

“Tunatuma rambirambi zetu kwa Gavana wa zamani wa Meru Kiraitu Murungi na familia yake, kufuatia kifo cha bintiye Anita Kendi Murungi,” aliomboleza Rais Ruto.

Huku akisema kifo cha Kendi ni mkasa mkubwa na limeacha pengo kwa familia ya Murungi, Rais Ruto aliiombea faraja familia hiyo wakati huu mgumu wa maombolezi.

“Mawazo na maombi yetu  yako kwa familia ya Murungi, wakati huu mgumu. Tunawaombea nguvu familia, marafiki na wale wote wanaoomboleza nao,” aliongeza Rais Ruto.

Hata hivyo, familia hiyo haijaelezea chanzo cha kifo cha kendi, ambaye alikuwa kitinda mimba wa Gavana huyo wa zamani wa Meru.

Share This Article