Rais Yoweri Museveni ameahidi kwamba muhula wake wa saba alioanza rasmi leo utakuwa bora huku akijiwekea changamoto kubwa na akaahidi kipindi cha kazi nyingi na mageuzi ya kiuchumi.
Muda mfupi baada ya kuapishwa kwa muhula wake wa saba mfululizo wa urais, Museveni aliuita muhula huu mpya wa mwaka 2026 hadi 2031 kuwa “Kisanja no-sleep”.
Pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia vyama vya upinzani, hasa National Unity Platform, NUP na Forum for Democratic Change, FDC, akivishtumu kwa kutumia vurugu wakati wa uchaguzi wa hivi karibuni.
Rais alianza hotuba yake kwa kutoa shukrani kwa jinsi uchaguzi wa hivi karibuni ulifanyika kwa amani, ambapo chama chake kilishinda kwa kiwango kikubwa.
Alikipongeza chama chake cha National Resistance Movement, NRM kwa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, wabunge, wenyeviti wa wilaya na madiwani.
Museveni pia alitambua vyama vingine vya kisiasa kama Democratic Party, DP na Uganda People’s Congress, UPC, akitambua ushiriki wao bila kutumia vurugu.
Kwa upande mwingine, Museveni alikosoa NUP na FDC, akivishtumu kwa kushiriki vitendo vya vurugu wakati wa kipindi cha uchaguzi.
“Ninavipongeza vyama vingine kama DP, UPC na vingine vilivyoshiriki uchaguzi bila kutumia vurugu, tofauti na chama cha NUP na baadhi ya wanachama wa FDC waliokuwa wakitumia vurugu,” alisema.
Alisihi vyama vilivyo chini ya Inter-Party Organisation for Dialogue, IPOD kuweka miongozo wazi ya usimamizi wa uchaguzi, kwa kuzingatia sheria na katiba ya Uganda.