Taasisi ya Bandari yaomba bunge kuboresha vifaa vyao

Mkuu wa taasisi hiyo alisema wananalazimika kupeleka wanafunzi Tanzania, Philippines au Uingereza kwa mafunzo ya juu

Marion Bosire
2 Min Read

Taasisi ya mafunzo kuhusu bahari Bandari Maritime Academy, imeomba kamati ya bunge kuhusu uchukuzi na miundombinu kusaidia katika kuiboresha.

Kamati hiyo iliombwa kufanya hivyo kwa kufanikisha kutengwa kwa fedha za kuboresha vifaa vya maigizo vya mafunzo ili kuafikia viwango vya kimataifa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa taasisi hiyo Dkt. Erick Katana, alitoa ombi hilo wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya bunge katika taasisi hiyo kwa lengo la kutathmini uwezo wake wa miundombinu, kozi za masuala ya baharini zinazotolewa, pamoja na changamoto zinazoikabili.

Katana aliambia wabunge hao kwamba taasisi hiyo ina uwezo wa kuzalisha wahandisi wa baharini wa kiwango cha dunia, ila wanahitaji vifaa vya kisasa.

“Tunalazimika kupeleka wanafunzi wetu katika nchi nyingine kama Tanzania, Philippines au Uingereza kwa mafunzo ya juu,” alielezea Katana.

Alitoa mfano wa Kifaa cha kisasa cha “full-bridge mission simulator” alichosema ni muhimu katika taasisi hiyo ya Bandarikwani kinatoa mazingira ya kidijitali yanayowawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa changamoto halisi za kiutendaji.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo George Kariuki ambaye ni mbunge wa Ndia, alieleza kuridhishwa kwake kutokana na ongezeko la vijana wa Kenya wanaojiunga na mafunzo ya masuala ya baharini.

“Kama kamati, tutatafuta njia ya kuunga mkono taasisi hii,” alisema Kariuki.

Kamati hiyo pia ilikagua kituo cha Kituo cha Mafunzo na Uthibitishaji wa Uokoaji Baharini ambacho bado kinajengwa.

Share This Article