Ssemuwemba: Ukuaji wa Dijitali umechochea maendeleo Afrika Mashariki

Tom Mathinji
2 Min Read
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Annette Ssemuwemba.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayehusika na maswala ya Forodha, Biashara na Fedha Annette Ssemuwemba, amesema ukuaji wa dijitali umepiga jeki maendeleo katika kanda ya Afrika Mashariki.

Kulingana na Ssemuwemba, teknolojia ya dijitali imeimarisha mawasiliano, utekelezaji biashara na utoaji huduma, hatua ambayo imefanikisha hatua kubwa za maendeleo katika kanda hiyo.

“Wakati mifumo ya kidijitali inafanya kazi kati ya mataifa, biashara zitafika katika masoko mapya. Wakati wananchi wanapata huduma kupitia mtandaoni, uzalishaji huongezeka na gharama hupungua,” alisema Ssemuwemba.

Aidha, Katibu huyo alisema kupitia mradi wa Utangamano wa kidijitali kanda ya Afrika Mashariki (EARDIP), Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ushirikiano na Shirika la Kimaendeleo la IGAD, zinashirikiana kuimarisha uunganishaji wa kidijitali kati ya mataifa, kupiga jeki biashara ya kidijitali, kuboresha usalama wa mtandaoni na kuwiainisha sera za kidijitali.

“Mustakabali wa Afrika unapaswa kuwa jumuishi. Sote pamoja, serikali, taasisi za kikanda, sekta ya kibinafsi, washirika wa kimaendeleo na vyombo vya habari zinaweza buni kanda ambapo teknolojia ya dijitali inachochea maendeleo, inabuni fursa na kuimarisha maisha ya watu wake,” alidokeza Katibu huyo.

Ssemuwemba alisema hayo Alhamisi wakati wa mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Shirika la IGAD, kuhusu uhamasishaji wa mradi wa EARDIP, ulioandaliwa Jijini Nairobi, Kenya.

Mkutano huo uliwaleta pamoja wataalam, wadau na wanahabari kutoka mataifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na wenyeji Kenya, Tanzania, Sudan Kusini, Djibouti na Uganda miongoni mwa nchi zingine.

Share This Article