Safari maarufu ya “Two Rivers Cruise” ya Chongqing ilisafirisha abiria 974,000 katika robo ya kwanza ya 2026, hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Haya ni kulingana na takwimu za kituo cha safari cha Chongqing Cruise Center.
Ziara za usiku ndizo zilizoongoza, zikichangia wageni 801,000 sawa na asilimia 82.2 ya jumla, huku kiwango cha ujazo wa vyombo (load factor) kikiwa wastani wa asilimia 77.3. Safari za mchana zilivutia abiria 173,000 pekee, sawa na asilimia 17.8, zikiwa na load factor ya asilimia 27.7.
Wachambuzi wa sekta hiyo wanaeleza kuwa hali hiyo inachangiwa pakubwa na “utambulisho wa mandhari ya usiku” wa jiji hilo unaotambulika kimataifa. Kauli ya muda mrefu ya wenyeji kwamba “hujashuhudia Chongqing kikamilifu hadi majira usiku” imeenea miongoni mwa watalii wa ndani na wa kimataifa.
Vivutio kama majengo ya jadi ya nguzo yaliyopambwa kwa taa za Hongyadong, mandhari ya kisasa ya Raffles City, muunganiko unaong’aa wa mito Yangtze na Jialing, pamoja na maonyesho ya mwanga kwenye madaraja ya jiji, huunda taswira ya “8D megacity” inayowavutia wageni mahsusi kwa ajili ya mandhari ya wakati wa usiku.
“Meli ya usiku inatoa msisimko wa kuzama ndani yake ambapo taa, usanifu na maji ya mto huungana kwa namna ya kuvutia sana,” alisema mtalii kutoka mkoa wa Jiangsu. “Ndiyo maana watu wengi wanakuja Chongqing.”
Takwimu za msimu na demografia zinaithibitisha mwenendo huo. Robo ya kwanza hujumuisha likizo ya mwaka mpya na wiki ya sikukuu ya majira ya kuchipua (Mwaka Mpya wa Kichina), ambapo watalii wa kutoka nje ya jiji huwa wengi mno. Wengi hutumia wakati wao mchana kutembelea maeneo maarufu kama Hongyadong, mtaa wa Jiefangbei na mji wa kale wa Ciqikou, kisha huhitimisha siku kwa safari ya usiku ya mito miwili, ratiba inayolingana na mienendo ya likizo na kupunguza msongamano unaoshuhudiwa wakati wa mchana.
Waendeshaji wa shughuli za utalii huo pia wamewekeza zaidi kwenye vipindi vya usiku, kwa kuhusisha safari nyingi zaidi, uwezo mkubwa, na huduma za ziada kama chakula ndani ya meli na burudani za moja kwa moja.
“Wageni wako tayari kulipia zaidi matukio na shughuli bora za usiku,” alisema mwakilishi wa kituo cha safari, akibainisha kuwa soko hilo linaendelea kuongozwa na mahitaji ya usiku.
Mwezi Machi mwaka huu, kwa mfano, watalii kutoka Sichuan walikuwa wengi zaidi kwa asilimia 13.4, wakifuatiwa na Henan (4.2%), Shanxi (4.0%), Shaanxi (3.7%) na Hebei (3.6%) mtawalia. Wakazi wa Chongqing wenyewe walichangia asilimia 2.6 tu ya abiria wa mwezi huo, wakishika nafasi ya 13 miongoni mwa mikoa na manispaa zote, na hivyo kushuka nafasi tano kutoka Februari.
Kwa umri, Machi ilionyesha kuwa kundi la wageni wenye miaka 18–34 lilikuwa asilimia 29.6 (ongezeko la pointi 1.5 mwaka hadi mwaka); miaka 35–59 ikiwa asilimia 51.6 (punguzo la pointi 1.1); wenye miaka 60 na zaidi wakuwa asilimia 15.3 (punguzo la pointi 0.4); huku walio chini ya miaka 18 wakibaki thabiti kwa asilimia 3.5.
Ongezeko la jumla la asilimia 1.7, pamoja na umaarufu wa ziara za usiku, linaonyesha uimara wa mandhari ya usiku ya Chongqing kama kivutio cha utalii na mafanikio ya sekta kuhamia kwenye utoaji wa huduma zinazovutia zaidi, kituo cha safari kilisema.
Chanzo: iChongqing.info