China yaondolea mataifa ya Afrika ushuru isipokuwa Eswatini

Eswatini iliachwa nje ya mpango huo kwa sababu ya kudumisha uhusiano na kisiwa cha Taiwan.

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali ya China imeanza kutekeleza sera inayozipa nchi za Afrika ufikiaji wa bila malipo wa soko lake kwa muda wa miaka miwili ijayo, isipokuwa taifa la Eswatini.

Sera hiyo iliyoanza kutekelezwa rasmi Ijumaa Mei Mosi, 2026, inajiri wakati ambapo mshindani wa Uchina ambaye ni Marekani, anaendelea kutekeleza ushuru mpya chini ya Rais Donald Trump kama njia ya kujikinga.

Mkataba huu unahusu mataifa 20 yanayochukuliwa kuwa yenye chumi kubwa zaidi barani kama vile Afrika Kusini, Misri, Nigeria, Algeria pamoja na Kenya.

Mataifa 33 yanayoorodheshwa kama yasiyojiweza tayari yalikuwa yakifurahia mpango huo wa kuafikia soko la China bila ushuru na hivyo sasa mataiga 53 kati ya yote 54 ya bara la Afrika yanafurahia mpango huo.

Taifa la Eswatini liliachwa nje ya mpango huo kwa sababu ndilo pekee barani Afrika limedumisha uhusiano na kisiwa cha Taiwan.

Tume ya Ushuru wa Forodha ya Baraza la Serikali nchini China ilisema kuwa makubaliano hayo yatachochea maendeleo ya pamoja ya China na Afrika.

Shirika rasmi la habari la China, Xinhua, lilisema kuwa mzigo wa tani 24 za tufaha kutoka Afrika Kusini uliopitishwa forodha huko Shenzhen alfajiri ya Ijumaa ulikuwa sehemu ya kwanza ya bidhaa zilizoingia chini ya sera mpya ya kutolipiwa ushuru.

Kulingana na Xinhua, Wizara ya Biashara ya China ilisema kuwa sera hiyo itanufaisha hasa bidhaa za Afrika kama kakao kutoka Ivory Coast na Ghana, kahawa na parachichi kutoka Kenya, pamoja na matunda ya machungwa na divai kutoka Afrika Kusini, ambazo awali zilitozwa ushuru wa kati ya asilimia 8 hadi 30.

Kutokana na hatua hii, baadhi ya nchi zenye uchumi mkubwa barani Afrika zilisema zitatafuta masoko mapya kwa baadhi ya bidhaa zao zilizokuwa zikipelekwa Marekani baada ya utawala wa Trump kuweka ushuru wa kulipizana mwaka mmoja uliopita.

China tayari ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika, bara lenye watu bilioni 1.5 ambalo linatarajiwa karibu kuongezeka mara mbili hadi bilioni 2.5 kufikia mwaka 2050, kulingana na Umoja wa Mataifa, ambapo litakuwa na zaidi ya robo ya watu wote duniani.

Share This Article